WADAU wa Elimu Kata ya Mtambani wakiwemo Wataalamu wa Serikali ngazi ya Wilaya na Kata wamekutana katika Kituo cha Jamii cha Kujifunzia Ruvu JKT.
Wamekutana katika kituo hicho kwa lengo la kujadili namna ambayo kila mmoja atatoa mchango wake katika kuelimisha watu wazima.
Akizungumza kwenye kikao hicho, mwezeshaji kutoka Shirika la DVV International, Mateo Mwita amewataka wataalamu kutumia taaluma zao kuwasaidia wanaosoma Elimu ya Watu Wazima ili waweze kujipatia kipato katika shughuli zao za kila siku.
"Dhana ya Elimu ya Watu Wazima imebadilika siyo kusoma, kuandika na kuhesabu tu, bali tunakuja na dhana ya kuwajengea uwezo wananchi katika kujipatia kipato na kuwa na maisha bora" amesema Mateo.
Mateo amesema katika Kituo cha Jamii cha Ruvu JKT, pamoja na kufundishwa kusoma, kuandika na kuhesabu; pia ujuzi mbalimbali utafundishwa ikiwemo ujasiriamali, elimu ya kuweka na kukopa, ufugaji, uvuvi, kilimo na elimu kwa vijana wa bodaboda.
Vilevile, Mateo amesema wana lengo la kuanzisha kituo cha watoto ili kuwasaidia kina mama wanaokuja na watoto waweze kuwaacha kwenye kituo na wao waendelee na masomo bila usumbufu.
Afisa Elimu ya Watu Wazima, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mektilida Kahindi amesema kwa sasa wanaendelea na uandikishaji wa wanakisomo wa Elimu ya Watu Wazima ambao wataanza masomo Januari, 2024 na kwamba hadi sasa walioandikishwa ni 153 ambapo wanaume ni 27; na wanawake ni 126.
Kahindi amesema wanajamii ya Mtambani wana mwamko mkubwa wa kujielimisha; hivyo wenyeviti wa vitongoji waliohudhuria kikao hicho wanatakiwa wachukue hatua ya kukitangaza kituo kwa wananchi ili wengine wajiunge na wafaidike na kituo hicho.
Mshiriki wa kikao hicho ambae ni Mmwenyekiti wa kitongoji cha Said Domo, John Pili amesema kuwa kutokana na elimu waliyopewa na mikakati waliyopanga, kuna matarajio ya Wananchi wa Mtambani na Halmashauri kwa jumla kunufaika kwa wingi.
Pili alisema kuwa mwaka mmoja baadaye jamii itashuhudia mabadiliko makubwa kwa wanakisomo watakaojiunga na Elimu ya Watu Wazima kwani mambo mazuri yatafundishwa.
Kituo cha Jamii cha Kujifunzia cha Ruvu JKT kinadhaminiwa na Shirika la DVV International.
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.