Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Butamo Ndalahwa na watumishi wa Halmashauri hiyo wameshiriki kufanya usafi katika kituo cha afya Mlandizi pamoja na kutoa msaada kwenye vituo vya kulelea watoto.
Shughuli hizo ambazo zimefanyika katika mji mdogo wa Mlandizi ni kati ya vitu vilivyofanywa na Halmashauri hiyo katika maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru ambayo kilele ni Disemba tisa.
Akizungumza baada ya kufanya usafi na kugawa misaada kwa wanawake wajawazito waliokuwa wanapata huduma katika Kituo cha Afya Mlandizi Ndalahwa alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maboresho yanayoendelea kufanyika kwenye sekta ya afya.
Alisema uwepo wa dawa na watoa huduma kwenye kituo hicho imesaidia kwa kipindi cha mwaka mzima kutokuwa na taarifa za vifo kwa Mama na mtoto huku huduma nyingine zikiwa zimeboreka.
"Katika maadhimisho haya tuliamua kufika katika kituo hiki cha afya na kutembelea vituo vinavyolelea watoto Yatima na wanaotoka kwenye mazingira hatarishi ili tuwasikilize vikwazo wanavyokumbana navyo na Serikali ione namna ya kusaidia kutatua changamoto hizo" alisema Mkurugenzi huyo.
Mganga Mfawidhi wa kituo Cha afya Mlandizi Dk.Sebastian Misoji alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri kwa namna ya ufuatiliaji na kushiriki kutatua vikwazo jambo ambalo limesababisha kituo hicho kutoa huduma bora na kutokuwa na vifo vya mama na mtoto kwa mwaka mzima.
Akishukuru baada ya kupokea msaada Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto cha Upendo Erick Ouma alimshukuru Mkurugenzi kwa kukumbuka kituo hicho na kuwapatia msaada.
Ouma alisema kwasasa kituo hicho kina watoto 19 na wapo ambao wanasoma vyuo, sekondari na shule za msingi.
Vituo vilivyopatiwa misaada hiyo ni pamoja na Vijaliwa vingi, Upendo na Masjid Noor ambavyo vyote vipo ndani ya Mji mdogo wa Mlandizi vikiwalea watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi na yatima.
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.