MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala ameomba Serikali kuandaa sheria kali kwenye utoaji wa mikopo ya asilimia kumi ili kudhibiti wanaokwamisha kwa kutorejesha kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana Mjini Mlandizi baada ya kikao cha baraza la Madiwani Makala alisema baadhi ya vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo havijarejesha na hivyo kukwamisha wahitaji wengine kunufaika.
Alisema endapo zitawekwa sheria zitasaidia kuondoa vikwazo vilivyopo sasa ambavyo viasababisha vikundi vinavyohitaji kukwama kupatiwa fedha kuyokana na watu wachache ambao hawajarejesha.
Makala alisema kutokana na hali hiyo Halmashauri kwasasa imejipanga kuchukua hatua za makusudi kwa wadaiwa ambao wanakwamisha malengo ya Halmashauri ya kuwezesha makundi ya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu kupata mikopo kwa wakati.
"Mikopo hii ya asilimia kumi sio hisani anayekopa anatakiwa kurejesha ili wengine wanufaike, na Madiwani wasiwatetee hawa wanaodaiwa wasimamie taratibu ili malengo ya Halmashauri ya kuyawezesha makundi yanayolengwa yafikiwe" alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alisema wameshatoa maagizo kwa watendaji wa Kata kuhakikisha wanachukua hatua kwa vikundi vilivyokopa virejeshe fedha hizo lakini pia wametoa miongozo kwa Maofisa Maendeleo ya jamii kushughulikia suala hilo kwani linasababisha kuwepo kwa hoja kwa wakaguzi wa hesabu za ndani na nje.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ruth Mwelo alisema vikundi vinavyopata mikopo vinatakiwa kupata elimu kuhakikisha wanarejesha fedha za mikopo kwa kuweka benki na si kuwapatia watumishi wawarejeshee.
Alisema watumishi wanaosimamia urejeshaji wa mikopo hususani wa Maendeleo ya jamii ngazi ya kata wanatakiwa wahakikishe wanakuwa waadilifu, waaminifu kwa mujibu wa sheria kwa kufanya kazi kwa kufuta taratibu kwa kutopokea fedha za vikundi za marejesho kutoka kwenye vikundi.
"Hairuhusiwi mtu yeyote hata kama ni msimamizi wa mikopo kupewa fedha mkononi kwasababu baadhi yao wamekosa uaminifu kwa kurejesha fedha hizo benki na hivyo kufanya Halmashauri kupata hasara.
Na hii ya kuwapatia wataalamu imesababisha baadhi ya vikundi kuonekana bado vinadaiwa wakati fedha wamewakabidhi wataalamu jambo ambalo ni kinyume na taratibu" alisema
Ruth alisema wakati mwingine hali hiyo inasababisha Halmashauri kupata hasara pale fedha hizo zikiwa hazirejeshwi na wengine kukosa fursa ya kukopa.
Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za Jamii Josephine Gunda alisema wadaiwa wa mikopo ya Halmashauri wanatakiwa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili vikundi vingine vinavyohitaji kukopa vinufaike kwa wakati.
Gunda alisema ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo intakiwa kuwachukulia hatua ili kukomesha tabia hiyo ambayo inawanyima wengine kunufaika.
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.