Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha limewafukuza kazi watumishi wawili kwa tuhuma za kukiuka kanuni za utumishi wa Umma.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erasto Makala ameyaeleza hayo jana katika kikao cha Baraza hilo cha kawaida kilichofanyika katika Ofisi za Halmashauri hiyo ambapo alisema hatua hiyo ni moja ya kufikisha ujumbe kwa watumishi wasio waadilifu.
Makala alisema waliofukuzwa kazi ni pamoja na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Soga kata ya Soga Winnie Sambo ambaye anatuhumiwa kuhusika na upotevu wa vitabu 20 vya kukusanyia mapato.
Aidha Sambo anatuhumiwa kuhusika na upotevu wa fedha zaidi ya sh.Miln 3 ambazo zinadaiwa kutumika katika shughuli mbalimbali bila kufuata taratibu.
Mwingine ni Mwanaasha Yusuph Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Kwala ambaye anatuhumiwa kutumia zaidi ya sh. Miln 28 ambazo zilikuwa ni marejesho ya mikopo ya vikundi .
Kwa mujibu wa Makala Afisa Maendeleo huyo anadaiwa kutumia fedha hizo kwa ajili ya matibu fedha ambayo ilitakiwa irejeshwe ili iingie kwenye mzunguko wa kuwezesha vikundi vingine kukopa.
" Hawa watumishi wameenda kinyume na kanuni ya Utumishi ya 42 ya mwaka 2022 tumelazimika kuchukua hatua hii kwakua hatupendi kuona mambo haya yanatokea kwenye Halmashauri yetu kila mmoja anatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu " alisema.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Butamo Ndalahwa alisema wamejipanga kusimamia na kuchukua hatua maelekezo yote yaliyotolewa na Baraza la Madiwani.
Ndalahwa alisema hatua za kinidhamu na onyo dhidi ya watumishi waliotolewa maelekezo na Baraza hilo yatafanyiwa kazi kuhakikisha kunakuwa na utendaji mzuri katika kuondoa kero za wananchi wanaowatumikia.
Moha ya maelekezo yaliyotolewa katika Baraza hilo ni pamoja na Mkaguzi wa ndani wa hesabu za Serikali kifika kwenye vijiji kukagua matumizi na mapato.
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.