KIBAHA DC YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 29.3
Halmashauri ya Wilaya ya kibaha Mkoani Pwani,imepitisha mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya Tsh 29,388,131,372.60 kwenye kikao cha baraza maalum la Madiwani lililofanyika kwenye ukumbi wa wazee Mlandizi.
Akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mhe. Mansour Kisebengo alisema kuwa lengo la kikao ni kupitia na kupitisha bajeti ya mwaka 2019/2020 itakayotoa mwanga wa nini kimepangwa kufanyika kwa mustakabali wa maendeleo ya Kibaha Vijijini.
Mwenyekiti amesema Kati ya fedha zilizotengwa kiasi cha Tshs. 1,986,514,976.40 ni makusanyo ya ndani, Tshs. 1,022,836,000.00 ni makusanyo yatokanayo na Mfuko wa Afya wa Jamii, ada, Bima na malipo ya papo kwa papo, Tshs, 23,509,899,027.94 ni Mishahara ya Watumishi, Tshs.1,015,631,091.26 ni matumizi ya kawaida na Tshs. 1,853,250,277.00 ni miradi ya maendeleo.
Kisebengo alisema Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/2020 umeandaliwa kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano awamu ya pili unaolenga Uchumi wa Viwanda, Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Sheria ya Bajeti, sura 439 na kanuni zake na Masuala yaliyosisitizwa katika mwongozo wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/2020.
Mwenyekiti ametaja vipaombele kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kuwa ni kuendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya,elimu ,utawala na kusimamia mpango wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.
Akiongea Wakati wa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Kibaha Butamo Ndalahwa amesema atasimamia mapato ipasavyo na kuwataka watendaji wote wa halmashauri pamoja na madiwani kutoa ushirikiano kwenye swala zima la kukusanya mapato.
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.